Habari | Afya | Makala | Magazeti | Michezo | Burudani | Teknolojia | Mapenzi

Lema Amtembelea Sugu Gerezani Awapa Neno Familia Yake


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amemtembelea gerezani mbunge mwenzake wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na kuifariji familia.

Lema ameieleza familia ya Sugu kuwa kukaa kwake mahabusu kumetokana na kuwatetea wananchi wa Mbeya na Tanzania kwa jumla na kwamba wabunge wengi wa upinzani wapo kwenye hesabu za kupelekwa gerezani, hivyo hawana sababu ya kunung’unika.

Mbunge huyo na mwingine wa Tandahimba (CUF), Katani Katani wakiongozwa na mwenyeji wao mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda waliitembelea pia familia ya Sugu eneo la Sae, Mbeya.

Kabla ya kwenda nyumbani kwa mama mzazi wa Sugu, Desderia Mbilinyi, wabunge hao walikwenda Gereza Kuu la Ruanda jijini hapa kuwajulia hali Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga ambao wapo mahabusu baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya wakikabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Lema alisema wamewakuta Sugu na Masonga wakiwa wazima, wenye afya njema na furaha, huku wakibainisha kwamba kukaa kwao mahabusu kumewapa ujasiri katika harakati za kisiasa.

“Mama sasa wewe unasikitika nini, wewe ni mama wa shujaa unalia nini? Kweli jela ni kubaya, lakini si kubaya kama umekwenda kwa sababu za kupigania haki za wananchi. Sugu hajaua, hajaiba televisheni wala hajabaka, hivyo mama wewe hapa inuka tembea kifua mbele kwamba mwanao yupo gerezani kwa sababu anatetea haki za wananchi, hii ni heshima kubwa sana mama yangu,” alisema Lema.

Lema alisema Sugu alishajitabiria kukaa gerezani kupitia nyimbo zake, na kweli sasa yupo gerezani.

“Lakini jua kwamba kuna siku, na kuna mwisho. Haya ni mapambano ya kiukombozi na ukiona hivi jua ukombozi umekaribia,” alisema.

Lema ambaye mara kadhaa amekaa mahabusu alisema kwa mpinzani kukaa gerezani au kufunguliwa kesi kunampa hekima, busara, kujenga mshikamono, moyo unaimarishwa na anakuwa na nguvu kubwa akitoka, hivyo anatamani na wabunge wengine wa upinzani wote wawekwe mahabusu ili wakapate ujasiri wa kuwapigania Watanzania.

Mbunge Katani alisema suala la Sugu na Masonga kukaa mahabusu kwake haoni kama ni kitu cha kushangaza bali kinampa faraja akiamini wakitoka huko watakuwa wamebadilika na kujazwa na ujasiri wa kuendeleza harakati za kuwapigania Watanzania.

Mbunge Sophia alisema, “Tunajua wananchi wana hasira kuona mbunge wetu yupo ndani kwa kunyimwa dhamana, lakini bado tunasisitiza waendelee kuwa watulivu.”

Akizungumza na wabunge hao, mama yake Sugu alisema ni jambo linalomnyima usingizi kuona mwanaye yupo mahabusu, lakini anajipa matumaini kwa kuwa mbunge huyo alianza harakati za kuwasemea wananchi akiwa bado mtoto mdogo.

“Inauma sana mwanangu kukaa kule, lakini anatetea haki za binadamu wenzake na nafikiri anachotenda ni halali kabisa hakuna tofauti. Mwanangu alitabiri mengi tangu yupo hapa nyumbani akiwa mtoto mdogo anaimba nyimbo, anatabiri matatizo ya nchi kwa hiyo hatushangai sana.”

Alisema, “Hata Lema na wenzake hapa wananihamasisha, hivyo sioni kama amefanya kitu cha ajabu yule (Sugu) ndivyo alivyo tangu utoto wake, ndiyo maana tukamuita Joseph maana yake ni mfanyakazi bora.” 
Reactions:

Post a Comment

[facebook][blogger]

EYOPAH

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget