Habari | Afya | Makala | Magazeti | Michezo | Burudani | Teknolojia | Mapenzi

NBS Yatoa Onyo Matumizi Mabaya ya Takwimu za Taifa


Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amesema takwimu za Taifa lazima ziheshimiwe na si kila mtu anastahili kuzitoa.

Dk Chuwa alisema hayo jana katika kipindi maalumu cha miaka miwili ya Rais John Magufuli kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Azam.

Alisema kazi ya kutangaza takwimu katika nchi zilizoendelea hufanywa na wataalamu na si kila mtu anapojisikia.

“Wenzetu wa Marekani, si rahisi kwa mtu yeyote kutangaza takwimu za Taifa au hata kumkuta akirandaranda maeneo zilipo ofisi za Taifa za takwimu,” alisema Dk Chuwa.

“Hata sisi Tanzania, inawezekana kazi ya kusambaza takwimu ikafanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pekee kwa sababu wataalamu tunao wa kutosha,” alisema.

Kauli ya Dk Chuwa imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kukosoa takwimu za Aprili na Juni zilizotolewa na Serikali kwamba hazikuwa sahihi.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini alisema takwimu za Serikali kuhusu kasi ya ukuaji wa uchumi katika robo ya pili ya mwaka ni tofauti na ukokotozi kwa kanuni za kiuchumi.

“Hatujatafuta takwimu nyingine, hizi ni taarifa zilezile zilizotolewa na BoT (Benki Kuu ya Tanzania)na NBS lakini ukikokotoa utaona uchumi unasinyaa badala ya kukua na hali ikiendelea hivi hadi Juni mwakani kutakuwa hakuna uchumi mwakani,” alikaririwa Zitto.

Katika kipindi hicho maalumu cha miaka miwili ya Rais John Magufuli, Kamishna wa Mapato ya Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Elijah Mwandumbya alisema katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imesajili biashara mpya 289,000.

Alisema jumla ya biashara 20,000 zilifungwa kutokana na kutoendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kulipa kodi stahiki na si kutokana na mazingira magumu ya biashara kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

“Tulisajili biashara nyingi 2016/17, hii ni kutokana na jitihada ya Serikali katika kuhakikisha inaboresha mazingira ya uwekezaji nchini,” alisema Mwandubya.

Alisema katika jitihada za kuendelea kuwavutia wawekezaji wengi zaidi, TRA tangu Novemba Mosi ilianzisha utaratibu wa msamaha wa kodi kwa miezi mitatu kwa biashara mpya.

Alisema jitihada hizo zinalenga kuongeza idadi ya walipa kodi ambao kwa sasa ni milioni 2.5 kati ya vijana 21 milioni wenye nguvu za kufanya kazi, kwa mujibu wa NBS

Reactions:

Post a Comment

[facebook][blogger]

EYOPAH

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget